Chama cha Wananchi (CUF) kimesema katibu wake mkuu, Maalim Seif Sharif
Hamad leo atakwenda katika Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC)
kuwashtaki viongozi wa Serikali kwa madai walitumia mamlaka yao vibaya
wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kisha kuwatesa, kuwakamata na
kuwapiga wafuasi wa chama hicho bila makosa.
Chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar, kimesema taratibu zote za
kufungua mashtaka hayo zimeshakamilika, ikiwa ni pamoja na kuweka
wakili.
Mei 22 mwaka huu, chama hicho kilizindua ripoti yake ya uvunjwaji wa
haki za binadamu Zanzibar wakati wa uchaguzi huo na kutangaza azma yake
ya kwenda ICC kuwashtaki Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mkuu wa
Jeshi la Polisi (IGP).
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Katibu Mkuu wa chama
hicho Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema mpango huo umekamilika na
Maalim Seif ambaye yuko nje ya nchi kwa ziara ya kueleza alichodai
‘figisufigisu’ zilizotokea katika uchaguzi mkuu, ataweka wazi kila kitu
kilichotokea na jinsi ukiukwaji wa demokrasia ulivyoshika kasi nchini.
Mazrui alimtuhumu IGP Mangu kuwa anatumiwa na CCM kuwakamata viongozi wa
CUF ili wasitimize azma yao ya kueleza ukweli wa yaliyotokea katika
uchaguzi, huku akimtaka afute azma yake ya kumkamata Maalim Seif kwa
maelezo kuwa “ataitumbukiza Zanzibar kwenye machafuko”.
Siku tano zilizopita, IGP Mangu wakati akihojiwa na Azam TV alisema
Jeshi la Polisi wakati wowote litamburuza mahakamani Maalim Seif kwa
kuhamasisha uchochezi Zanzibar. Iwapo CUF itatekeleza azima hiyo,
itakuwa tukio la kwanza kwa Tanzania kupeleka viongozi wake kwenye
mahakama hiyo.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na naibu wake, William Ruto wameshafikishwa
huko, lakini kesi dhidi yao zilikosa nguvu na kuondolewa.
Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC),
Salim Jecha Salim alifuta matokeo ya rais, wawakilishi na madiwani
Oktoba 28, mwaka jana siku ambayo alitakiwa atangaze mshindi wa mbio za
urais.
CUF ilidai kuwa ilishinda uchaguzi huo na Jecha alipotangaza uchaguzi wa
marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu, chama hicho kilijitoa na hivyo
CCM kushinda viti vyote.
Mazrui ambaye aliambatana na viongozi wengine wa chama hicho alisema:
“Mpango wa kuishawishi dunia kuwachukulia hatua wahusika wote wa
ukiukwaji wa haki za binadamu na uvunjwaji wa demokrasia uko palepale,
hautasitishwa kwa vitisho vyovyote.
“Lengo ni kuhakikisha unyama dhidi ya raia wasio na hatia unakomeshwa
na uzingatiwaji wa sheria za nchi unatamalaki. Tunawaambia polisi kuwa
tumechoshwa na figisufigisu maana zitazaa timbwiri.”
Mazrui alisema wanaotaka kuzuia mpango wa CUF kueleza ukweli na kwenda
ICC, wanaandaa utaratibu wa kumkamata Maalim Seif aliyedai; “Ni kipenzi
cha Wazanzibari”, akisisitiza kuwa jambo hilo ni hatari kwa sababu
litaivuruga Zanzibar.
Akifafanua zaidi kile alichokiita mikakati ya CCM kupitia kwa IGP Mangu
kuficha ukweli, Mazrui alidai kuwa polisi wamekuwa wakiwakamata
wanachama wa CUF mara kwa mara.
"Niongeavyo hapa wanachama zaidi ya 400 wa CUF wamekamatwa na wengine wapo nje wa dhamana,” alisema.
Alisema ni jambo la ajabu kuona IGP Mangu akishindwa kutoa kauli yoyote
baada ya Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DDCI), Salum Msangi
kuwatishia mawakili kuwatetea wananchi wanaokamatwa kwa tuhuma
mbalimbali.
Alisema viongozi wa CUF hawatatishwa wala kunyamazishwa katika kudai
haki ya ushindi wa Wazanzibari kutokana na uamuzi wao wa uchaguzi mkuu.
Katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa
chama hicho, Shaweji Mketto alisema endapo IGP Mangu ataendelea
kuwatisha viongozi wa CUF, watajipanga kwenda kumtembelea ofisini kwake.
IGP Mangu ajibu
Alipoulizwa kuhusu kauli za CUF, IGP Mangu alisema tayari ameshatoa
msimamo wa Jeshi la Polisi na walichokifanya viongozi wa chama hicho ni
kumjibu tu.
“Ukipendwa sana ukafanya uhalifu tukuache? Tukikutuhumu unafanya makosa
tutakukamata hatuwezi kuogopa umaarufu wako,” alisema huku akisisitiza
kuwa jalada kuhusu Maalim Seif lipo kwa DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka).
“Umesema hao CUF wamesema kuna wanachama wao wamekamatwa, sasa
wamekueleza hao wanachama ni kina nani?… kama wamekamatiwa Zanzibar wapo
maofisa wa polisi wa mikoa wanaoweza kuzungumzia hilo huko Zanzibar.”
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema: “CCM hatuwezi
kujiingiza katika hoja za IGP na CUF tumewaachia wenyewe. Kwa sasa tupo
katika maandalizi ya kuhakikisha Rais (John) Magufuli anashinda kwa
kishindo kuwa mwenyekiti wa CCM.” Alisema chama hicho hakina sababu ya
kutumia Jeshi la Polisi kukandamiza wanachama na viongozi wa CUF.