Baada ya miaka 18 mfululizo ya kutamba na bendi za Dar es Salaam, hatimaye Ally Chocky ameamua kwenda Mwanza na kujiunga na bendi ya Super Kamanyola yenye maskani yake Villa Park Resort.
Ally Chocky mwimbaji aliyetamba na bendi za Twanga Pepeta, Extra Bongo, Double Extra, Mchinga Generation na TOT Plus, amedai kuwa sasa ni wakati muafaka wa kubadili upepo na ndiyo maana amekubali kwenda Mwanza kuitumikia Super Kamanyola.
Mwimbaji huyo aliyeanza kutengeneza jina miaka ya 90 kupitia bendi za Lola Afrika, Bantu Group, Washirika Stars na MK Beats, aliwahi kuchukua hatua kama hii ya kubadili upepo miaka ya nyuma kwa kwenda nchini Kenya na kukaa kwa miaka kadhaa kabla ya kurejea Dar es Salaam mwaka 2000 na kujiunga na Twanga Pepeta.
Chocky ambaye alikuwa msanii huru tangu alipomaliza mkataba wake Twanga Pepeta mwezi April mwaka huu, amesema ataanza rasmi kuitumikia Super Kamanyola wiki ijayo.
Amedai ndani ya kibarua chake hicho kipya, itadumbukizwa program ya nyimbo zake alizotunga akiwa na bendi mbali mbali, hatua itakayoenda sambamba na utengenezaji wa nyimbo mpya.