MWENYEKITI
wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais mstaafu Jakaya Kikwete,
amekata mzizi wa fitna kwa kutangaza rasmi kuwa Mkutano Mkuu Maalumu wa
CCM, utakaofanyika mjini Dodoma kesho utafanya kazi moja tu ya kumchagua
Rais John Magufuli kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho.
Kikwete alisema hayo alipofungua kikao cha Kamati Kuu ya CCM kwenye
ukumbi wa White House, makao makuu ya CCM, mjini hapa jana. Kauli hiyo
ya Kikwete inamaliza minong’ono ya muda kuwa hapangekuwa na kupokezana
kijiti katika mkutano huo.
Pia kauli hiyo imezima madai kwamba kungekuwa na mchujo katika uchaguzi
wa Mwenyekiti, ambapo majina hadi matano yangependekezwa na Kamati Kuu
na kupelekwa katika Halmashauri Kuu ambayo ingekata mawili na kupeleka
matatu kwenye Mkutano Mkuu Maalumu, ili yapigiwe kura kumchagua
Mwenyekiti.
“Ajenda yetu kubwa leo (jana) ni moja tu; nayo ni kupendekeza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ili
nayo Halmashauri Kuu ya Taifa ipendekeze kwa Mkutano Mkuu wa CCM ili
achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa CCM,” alisema Kikwete kwenye ufunguzi huo
wa Kamati Kuu, akitumia dakika tano tu, kisha wajumbe wakaendelea na
ajenda. Rais Magufuli alichaguliwa kuongoza Tanzania Oktoba mwaka jana.
Katika hotuba yake hiyo ya jana, Kikwete aliwajia juu ‘wafitini’ walioombea chama hicho kife katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Alisema “Wapo watu walidhani CCM ingekufa na walishajiandaa na salamu za
rambirambi. Walidhani wataibuka. Hawakuibuka na hawataibuka kamwe.”
Kikwete aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa kilikuwa kikao chake cha
mwisho cha Kamati Kuu, kauli iliyobainisha wazi kuwa anang’atuka
kumwachia kijiti Rais Magufuli kuongoza chama.
Alisema amekuwa Mwenyekiti wa Chama kwa miaka 10, hivyo aliwashukuru
wajumbe wa Kamati Kuu kwa kumsaidia katika kipindi chote hicho huku
akisisitiza; “Bila msaada wenu CCM isingekuwa imara kama ilivyo hivi
leo.”
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Rais Magufuli alikuwa
akifahamika kama Tingatinga na kwenye mikutano kadhaa, Rais mstaafu
Kikwete aliweza kumuita kwa jina hilo.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa CCM, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete jana
alikagua ukumbi wa mikutano wa CCM na kuoneshwa sehemu mbalimbali ambapo
alisema ameridhika na maandalizi ya mkutano kwamba yanaenda vyema.
Maeneo mengine aliyotembelea ni mabanda ya mama na baba lishe, sehemu za
kutolea huduma za Benki na mabanda ya maonesho ya wajasiriamali.
Katika ziara hiyo aliambatana na Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana, makamu
Mwenyekiti Bara, Phillip Mangula, waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na
Michezo Nape Nnauye, msemaji wa CCM Christopher Ole sendeka, naibu
katibu mkuu wa CCM Bara Rajab Luhwavi na wajumbe wa Kamati Kuu Pindi
Chana na Mohamed Seif Khatib. Wajumbe wa mkutano Mkuu maalum wa CCm
walianza kuwasili jana na wengine wengi wanatarajiwa leo.
Title :
KIKWETE AWAPA MADONGO LIVE! KUNA WATU WALIDHANI ETI CCM ITAKUFA.
Description : MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais mstaafu Jakaya Kikwete, amekata mzizi wa fitna kwa kutangaza rasmi kuwa Mkutano...
Rating :
5